JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

TPC KUSHIRIKIANA NA POSTA ZA AFRIKA


Shirika la Posta Tanzania limejidhatiti kushirikiana na Posta nyingine Barani Afrika hususani katika huduma za Biashara Mtandao “E-Commerce” pamoja na huduma za Usafirishaji kupitia miundombinu iliyoboreshwa na Tanzania katika kurahisisha huduma kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Postamasta Mkuu Bw. Maharage Chande wakati akizungumza na Postamasta wakuu wa nchi za Zambia, Zimbabwe, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo pamoja na Mdau wa Sekta ya Posta ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ship2MyID ya Marekani, katika Ofisi ya Postamasta Mkuu iliyopo Makao Makuu ya PAPU, jijini Arusha.

Aidha, Bw. Maharage ameelezea maendeleo ya kiteknolojia yaliyofanywa na Shirika la Posta Tanzania likiwemo Duka Mtandao linalowezesha wananchi Duniani kote kuuza, kutangaza na kununua bidhaa pia kufikishiwa popote pale walipo.

Akizungumza wakati akiwa na Viongozi hao Bw. Maharage ameeleza kuwa, kwa sasa Tanzania imeboresha miundombinu ya usafirishaji kupitia Shirika la Ndege ATCL ambapo mizigo inaweza kusafirishwa kwenda nchi nyingi Duniani kwa uharaka zaidi kwani safari za ndege zimeongezeka kuelekea Dubai, China na Mumbai kwa takribani mara tatu kwa wiki. 

Kwa upande wa viongozi hao wameridhia uwepo wa mashirikiano ya kibiashara na Posta Tanzania na kupongeza jitihada za Tanzania kuendelea kuweka miundombinu wezeshi kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa huduma za Posta kwa urahisi, uharaka na usalama zaidi.

Postamasta Mkuu amekutana na viongozi hao katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) huku Tanzania ikiwa mwenyeji wa Mkutano huo ulioanza Juni 3 hadi 14 , 2024 jijini Arusha yalipo Makao Makuu ya Ofisi za PAPU.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA