JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

TPC WAASWA KUUELEWA MPANGO MKAKATI 9


Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Amwesiga Kamihanda, kwa niaba ya Postamasta Mkuu, Bw. Macrice Mbodo, amewaasa wafanyakazi wa Shirika kuongeza bidii katika kuuelewa na kuutekeleza Mpango Mkakati wa Tisa ili kuyaishi malengo ya Shirika na kuendelea kutoa huduma bora kulingana na mahitaji ya sasa ya wananchi na kuleta tija kwa Taifa.

Ameyasema hayo tarehe 01 Mei, 2026 mkoani Njombe, wakati wa hafla fupi ya kumpongeza Mfanyakazi Hodari Kitaifa, iliyofanyika sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Wakati wa hafla hiyo, Bw. Kamihanda alisisitiza kuwa katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia yanayoendelea kwa kasi duniani, Posta haina budi kujipanga upya kila wakati ili kuhakikisha linaendelea kuwa la kisasa, shindani na la kuaminika.

Aidha, aliwahimiza wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na kutumia ubunifu katika utoaji wa huduma ili kuongeza mapato na ufanisi wa Shirika.

Pia, alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mfanyakazi Hodari Kitaifa, Bw. Gershom Timoth Mbago, akieleza kuwa utendaji wake bora ni kielelezo cha ari, uwajibikaji na ubunifu unaohitajika katika kufanikisha malengo ya Shirika, na kwamba mfano huo utaamsha ari mpya kwa wafanyakazi wengine.

 

Imetolewa na:

IKitengo cha Mawasiliano

Shirika la Posta Tanzania


© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA