Habari
TPC YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MUUNGANO
Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeshiriki kwa mafanikio katika Maonesho ya huduma zake kwenye viwanja vya Mao Zedong, Zanzibar wakati wa kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ushiriki huu wa TPC ulitoa fursa ya kipekee kuonyesha huduma zinazotolewa na Shirika hasa kipindi hiki ambacho Shirika lipo katika mageuzi makubwa ya kutoa huduma za kidijitali na ikizingatiwa kuwa Shirika la Posta ni Shirika la Muungano.
Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Riziki Pembe Juma, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mh.Waziri alitembelea banda la Shirika la Posta Tanzania ambapo alipokea maelezo ya kina kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika kwa wananchi wa Tanzania kutoka kwa Bw. Ferdinand Kabyemela, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo, aliyemwakilisha Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo.
Moja ya huduma zilizomvutia Mhe Waziri ni huduma ya Swifpack inayotolewa na Shirika ambayo imekuja kama mkombozi wa huduma za usafiri na usafirishaji unaounganisha biashara na wateja kwa haraka, usalama, na bei nafuu. Mhe. Waziri alionyesha furaha yake na kupongeza juhudi za Shirika katika kuleta ubunifu wa kidijitali ambao unakidhi mahitaji halisi ya wafanyabiashara na wananchi wa kawaida wa Tanzania Bara na Visiwani.
Katika maadhimisho hayo Bw. Kabyemela aliambatana na Meneja Mkaazi Zanzibar Bi. Halima Hamad na Mkuu wa Mawasiliano na Masuala ya Posta Kimataifa Bw. Elia Madulesi. Itakumbukwa kuwa Shirika la Posta ni Shirika la Muungano linalotoa huduma pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

