Habari
UMOJA WA POSTA DUNIANI YAITUNUKU POSTA
Shirika la Posta Tanzania limetunukiwa Cheti cha Usalama cha Kimataifa (S58 & S59) kutoka Umoja wa Posta Duniani (UPU), kufuatia mafanikio katika zoezi la tathmini ya usalama wa mifumo, miundombinu na taratibu za utoaji huduma lililokamilika tarehe 7 Novemba 2025.
Cheti hicho cha Daraja “A” (tuzo ya dhahabu) kimetolewa rasmi leo, tarehe 24 Novemba 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani UPU, Bw. Masahiko Metoki, mara baada ya timu ya wataalamu wa UPU kufanya ukaguzi wa kina wa wiki moja uliolenga kuhakiki viwango vya usalama wa Shirika katika kulinda mizigo, barua na taarifa nyeti zinazopitia katika mnyororo wa huduma za posta.
Katika zoezi hilo la tathmini, Shirika la Posta Tanzania limepata alama 598 kati ya 640, likitimiza kwa ufanisi vigezo vyote vya kupewa cheti hicho cha heshima kinachotolewa kwa taasisi za posta zinazofikia viwango vya juu vya usalama wa kimataifa.
Wakipokea cheti hicho kwa niaba ya Shirika, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo, Bi. Caroline Kanuti, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika, S.P. Mathias Kipeta, wameishukuru UPU kwa kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Shirika katika kuimarisha usalama wa huduma zake, na kuahidi kuendeleza maboresho endelevu katika mifumo na miundombinu ya Shirika.
Aidha, wataalamu wa UPU waliwasilisha mapendekezo ya kuongeza ufanisi zaidi katika maeneo ya udhibiti wa mizigo, ufuatiliaji wa usafirishaji wa barua na vifurushi, pamoja na uboreshaji wa vituo vya kuchakata mizigo (Office of Exchange), ili kuhakikisha huduma bora, salama na za kisasa.
Kupitia mafanikio haya, Posta Tanzania sasa imeorodheshwa rasmi miongoni mwa waendeshaji wa huduma za posta duniani waliotunukiwa cheti cha usalama na UPU, hatua inayoliweka Shirika katika nafasi ya juu kimataifa, na kuimarisha uaminifu, ushindani na ubora wa huduma kwa wananchi na wateja wa kimataifa.

Kushoto Bi. Caroline Kanuti kwa niaba ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na Kulia S.P. Mathias Kipeta, Mkuu wa Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika la Posta Tanzania.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

