Habari
BODI YA UPU QSF YAFANYA KIKAO CHA 95
Mkutano wa 95 wa Bodi ya Mfuko wa Ubora wa Huduma wa Umoja wa Posta Duniani( UPU Quality of Service Fund -QSF) umefanyika jijini Baku, Azerbaijan kuanzia Julai 14 hadi 18, 2026, ukiwakutanisha wajumbe kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha mitandao na ubora wa huduma za posta duniani.

Mhandisi Clarence Ichwekeleza, kutoka Shirika la Posta Tanzania ni Mjumbe wa Bodi hiyo akiwakilisha Tanzania na Bara la Afrika katika Bodi hiyo yenye wajumbe 11 kutoka nchi mbalimbali duniani ameshiriki kikao hicho.
Katika kikao hicho, wajumbe walifanya tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Magari ya usafirishaji wa Barua na Vifurushi unaotekelezwa na Shirika la Posta la Azerbaijan(Azerpost ) kwa ufadhili wa Bodi hiyo, ambapo matokeo yalionesha mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma.
Tathmini hiyo ilibaini kuwa kiwango cha utoaji huduma kimeongezeka kutoka 59% mwaka 2024 hadi kufikia 75% mwaka 2026, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji.

Kutokana na mafanikio hayo na umuhimu wa miradi inayotekelezwa katika nchi wanachama, Bodi ya QSF imeazimia kuwa Mkutano wa 97 wa Bodi ufanyike nchini Tanzania.
Mkutano huo utatoa fursa kwa wajumbe kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za usafirishaji wa ndani ya miji (Intra-town Service Delivery Project) unaotekelezwa na Shirika la Posta Tanzania, ukiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi, kasi na ubora wa huduma za posta nchini.

Uamuzi wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaonesha imani ya Bodi ya QSF katika juhudi zinazoendelea kufanywa na Shirika la Posta Tanzania katika kuboresha huduma za posta na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo kimataifa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

