JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

MKUTANO MKUU WA NNE WA UPU


Tanzania Washiriki Mkutano wa Nne wa Dharura wa UPU nchini Saudi Arabia kujadili maendeleo ya sekta ya posta duniani na mageuzi ya kidijitali. Waziri Nape Nnauye anaongoza ujumbe, akisisitiza dhamira ya Tanzania. Mazungumzo ya pande mbili na Oman pia yanajadili miradi na uunganishaji wa kidijitali.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Mb) Ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano Mkuu wa nne wa Dharura uliofanyika Riyadh nchini Saudi Arabia kuanzia tarehe 01/10/2023 hadi 05/10/2023 ambao umeandaliwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) huku ukihusisha nchi wanachama 192 wa Umoja wa Posta Duniani.

Mkutano huo una lengo la kuwajumuisha watoa huduma binafsi katika Umoja wa Posta Duniani kushughulikia masuala ya maendeleo ya TEHAMA hasa katika utoaji na urahisishaji wa huduma za Posta Duniani.

Katika mkutano huo Mhe. Nape amesisitiza umuhimu wa kuweka kipaumbele katika kukuza Sekta ya Posta duniani huku akitilia mkazo juhudi za Tanzania za kuongeza ufanisi wa Huduma za Posta chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia anaunga mkono mageuzi ya kidijitali yanayoendelea katika Sekta ya Posta ya Tanzania.

Mhe. Nape ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Bi. Khadija Khamis Rajab, pamoja na maafisa kutoka Wizarani.

Aidha, Shirika la Posta Tanzania na Posta Oman zilitumia nafasi hiyo kuwa na kikao cha pembeni kujadili masuala mbalimbali ya kibiashara ikiwemo utekelezaji wa Makubaliano ya kibiashara (MoU) kati ya nchi hizi mbili pamoja na miradi iliyopo baina ya nchi hizi ambayo ilitiwa saini mwaka 2022, nchini Tanzania ikiwa na lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za Posta nchini Tanzania, Oman pamoja na Ukanda wa Afrika Mashariki.

Sambamba na hilo nchi hizi mbili zilijadili namna bora ya kuimarisha na kuendeleza Mashirikiano hayo katika Nyanja za biashara mtandao ili kujenga miundombinu ya kuwezesha uhifadhi na usambazaji wa bidhaa, utumaji na upokeaji fedha katika mfumo wa Posta pamoja na uchapishaji wa stempu ya pamoja

Vilevile nchi hizi zimejadili masuala ya kufanya upembuzi yakinifu (Feasibility Study) kwa ajili ya uanzishaji wa Mradi utakaorahisisha biashara ya mtandao kutoka Tanzania hadi Kuunganisha nchi za Oman na zile za Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Kukamilisha uundaji wa mfumo wa ujumuishi wa kifedha wa UPU (IFS Cloud) ambao utarahisisha utumaji fedha kutoka Tanzania na Oman kupitia Mtandao wa Posta.

Shirika la Posta Tanzania limewakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Brigedia Jenerali Mstaafu Yohana Ocholla Mabongo akiambatana na Postamasta Mkuu Bw. Maharage Ally Chande, Mkurugenzi wa Huduma za Posta Ndg. Arubee Ngaruka, Mkurugenzi wa Biashara Mtandao na Huduma za Fedha Bw. Constantine Kasese.

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA