Habari
WAZIRI MKUU AKISIKILIZA MAELEZO YA PMG

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameonyesha kufurahishwa na mfumo wa anwani za makazi unavyorahisisha huduma za Posta hususani sekta ya usafirishaji.
Hayo yamejiri leo Jumamosi tarehe 8 Februari, 2025 alipotembelea banda la maonyesho la Shirika la Posta Tanzania akiwa na lengo la kujionea namna walivyojiandaa kuwafikia wananchi katika maadhimisho ya wiki ya Anwani za makazi Jijini Dodoma.
Majaliwa amepata nafasi ya kusikiliza maelezo kutoka kwa Postamasta Mkuu Macrice Mbodo namna Mfumo wa Anwani za Makazi unavyorahisisha huduma za usafirishaji kwa Shirika la Posta Tanzania.
Aidha, Postamasta mkuu ameelezea namna ambavyo vifaa saidizi vya kidijitali vijulikanavyo kwa jina la (Personal Digital Assistant-PDA) vinavyosaidia utendaji wa Shirika la Posta Tanzania kwa kupokea, kusafirisha na kufikisha taarifa za bidhaa kwa wateja.
Shirika la Posta Tanzania linashiriki Maonesho ya siku tatu ya Wiki ya Anwani za Makazi yaliyoanza Februari 6, 2025 hadi Februari 8, 2025 katika Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania