JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

WAZIRI SILAA AZINDUA RASMI BODI YA TPC


Mhe. Jerry William Silaa (Mb) Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amezindua rasmi Bodi ya Shirika la Posta Tanzania katika hafla iliyofanyika leo tarehe 18 Novemba, 2024 katika Ukumbi wa Bodi, Posta House, jijini Dar es Salaam.
 
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akiwemo Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu, Bw. Nicholas Merinyo Mkapa, Naibu Katibu Mkuu, na Bw. Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa Mawasiliano.
Bodi ya Wakurugenzi waliohudhuruia ni pamoja na Balozi Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Salim Milanzi, Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Toyi A. Ruvumbangu, Makamu mwenyekiti wa Bodi, Bw. Hassan O. Kitenge, Mjumbe, Bi. Caroline Kanuti, Mjumbe, Bw. Nura Mohamed Abubakari, Mjumbe, Bw. Matimbila I.Paul, Mjumbe na CPA Poriwoa A. Mbisse. Kwa upande wa Shirika Bw. Macrice D. Mbodo, Postamasta Mkuu pamoja na Menejiment ya Shirika walihudhuria uzinduzi huo.
 
Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi, Mhe. Jerry Silaa amesisitiza umuhimu wa Shirika la Posta Tanzania kuendana na maendeleo ya TEHAMA na mapinduzi ya viwanda ya sasa ili kuimarisha huduma zake na kuchangia zaidi katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini. Ametumia nafasi hii kuelekeza bodi kusimamia ubunifu katika huduma za Shirika ikiwemo matumizi bora ya TEHAMA. Kutekeleza miradi yenye tija kama vile, mradi wa maghala na duka mtandao. Kuhakikisha ushirikiano thabiti kati ya Bodi Menejimenti na Watumishi ili kuongeza ufanisi.

Katika tukio hilo, Mheshimiwa Silaa amewapongeza Mwenyekiti wa Bodi, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe wote wa Bodi kwa kuteuliwa kwao na amewataka kutumia ujuzi wao wa taaluma mbalimbali kuhakikisha Shirika linafikia malengo yake.
 
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amekabidhi rasmi majukumu kwa Mwenyekiti wa Bodi ambayo alikuwa akiyafanya wakati bodi hiyo haijateuliwa. Akikabidhi majukumu hayo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara na Bodi katika kutekeleza malengo ya Shirika. Pia amesema kuwa Wizara ipo tayari kutoa usaidizi utakaohitajika katika utekelezaji wa majukumu hayo.

Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Salim Milanzi, kwa upande wake ametoa shukrani kwa Serikali kwa imani kubwa iliyowekwa kwao na kuahidi kuwa Bodi itafanya kazi kwa bidii, weledi, na kuzingatia maadili ili kufanikisha malengo ya Shirika. Pia amesema kuwa Bodi hiyo itazingatia maelekezo ya Waziri na kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa tija.

Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo ameipongeza Bodi mpya kwa uteuzi wao amesema ujio wao umetupa nguvu mpya ya kusonga mbele zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Pia amesisitiza kuwa Menejimenti na watumishi wa Shirika wapo tayari kushirikiana kikamilifu na Bodi mpya ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, Bw. Mbodo ametoa shukrani kwa Katibu Mkuu wa Wizara Bw. Mohammed Abdulla kwa kusimamia majukumu ya Bodi kwa kipindi ambacho Shirika halikuwa na Bodi ya Wakurugenzi.
 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA