Habari
TUMEFUNGUA FURSA
Katika kuendelea kupanua huduma na kuongeza thamani kwa wateja wake, Shirika la Posta Tanzania limeingia katika ushirikiano na Vertex International Securities ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za uwekezaji kwa wananchi kupitia mtandao mpana wa Posta nchini. Ushirikiano huu umefungua milango kwa Watanzania wengi zaidi kushiriki katika fursa za uwekezaji ambazo hapo awali zilionekana kufikika kwa kundi dogo la watu.
Kupitia ushirikiano huo, wananchi wanaweza kupata taarifa na huduma zinazohusiana na uwekezaji kwa urahisi zaidi, huku wakinufaika na uwepo wa mtandao mkubwa wa ofisi za Posta unaofika katika maeneo mbalimbali nchini. Hatua hii inaunga mkono juhudi za kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha.
Mafanikio haya yanaonesha dhamira ya Shirika la Posta Tanzania ya kuendelea kubuni na kuanzisha ushirikiano wa kimkakati unaowanufaisha wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali. Kupitia huduma hizi, Posta imeendelea kuwa daraja muhimu linalounganisha wananchi na fursa mbalimbali za kiuchumi na kifedha.
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania.

